Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga,
Nyabaganga Taraba ameagiza uchunguzi ufanyike mara moja kubaini chanzo cha moto
ulioteketeza bweni la wasichana shule ya sekondari Bunambiyu.
Tukio hilo lilitokea leo Jumatatu saa 2 asubuhi
wakati wanafunzi hao wakiwa madarasani na kusababisha uharibifu wa vifaa vikiwemo
vitanda 12, magodoro 36 na mali zao zote.
Taraba pia amewataka wanafunzi katika shule hiyo iliyopo
kata ya Bunambiyu kutoa ushirikiano wa kawaida uchunguzi ukiendelea kufanyika
ili kubaini chanzo cha moto huo
Kwa mujibu wa mwalimu wa shule hiyo, Lameck
Manumbu pamoja na jitihada za wanafunzi na wanakijiji wa Bunambiyu kuzima moto
huo hawakufanikiwa kwani ulikuwa umeshika kasi na kuteketeza bweni hilo
linalotumiwa na wanafunzi wa kike 26.
Taraba akiwa katika eneo la tukio akiambatana na
Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya hiyo, Stephen Magoiga, baadhi ya
wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na wataalamu wa sekta mbali mbalimbali walifanya
tathimini ya awali na misaada kwa wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya na timu yake waliungana na Uongozi
wa Shule, Ungozi wa Kata na Kijiji na wananchi majirani na shule na walifanya
kikao cha kazi kutafuta chanzo cha moto na kutafakari hatua za haraka za
kuchukua.
Kwa kushirikiana na uongozi wa shule walianisha mahitaji
ya haraka kuwasaidia waathirika na kuwapatia makazi ya muda huku hatua za kuwanunulia
shuka zote pamoja na baadhi ya mahitaji zilifanyika.
Mkuu wa wilaya alihamasisha mchango wa papo ambapo
zilipatikana jumla ya sh. 272,000 ambazo walipewa waathirika na kila mmoja
alipata 10,000 kwa ajili ya mahitaji ya haraka wakati wakisubiri mahitaji mengine
ya awaida ili waendelee na masomo wakati wakiwasiliana na wazazi wao.






