Wednesday, June 14, 2017

ACACIA Waeleza Utata wa Usajili wa Kampuni Yao

Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia, imesema kuwa inafanya kazi nchini kwa misingi ya sheria na Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA) inatambua uwepo wake.

Kauli hiyo imekuja baada ya juzi taarifa ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa mchanga wa madini katika makontena yalizuiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi, kubainisha kuwa kampuni hiyo haina kibali na inafanya kazi kinyume na sheria.

Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jana pia imesema kuwa Acacia itafanya mkutano na wanahisa wake kesho kutoa ufafanuzi zaidi juu ya sakata zima.

Kampuni hiyo ilieleza kuwa migodi yake ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara inaendeshwa kisheria.

“Acacia inapenda kuthibitisha kwamba inaendelea kufanya kazi katika migodi yake mitatu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara.

“Migodi hii yote inamilikiwa na kuendeshwa na makampuni ambayo yamesajiliwa Tanzania kisheria; Bulyanhulu Gold Mine Limited, Pangea Minerals Limited na North Mara Gold Mine Limited ambayo yana leseni maalumu kwa kila mgodi,” inasomeka sehemu ya taarifa  ya Acacia ambayo tumeiweka hapo chini.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza: “Kampuni hizi zinamilikiwa na Acacia ambayo imesajiliwa nchini Uingereza ingawa umiliki huu si wa moja kwa moja (indirectly owned).

“Muundo huu ni wa uwazi, upo kisheria na huwekwa wazi katika taarifa zetu za hesabu za mwaka ambazo hukaguliwa kwa mujibu wa taratibu za kimataifa.”

Taarifa hiyo iliendelea kufafanua kwamba utaratibu huo wa umiliki uliwekwa wazi kwa CMA wakati Acacia ikijioredhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2011.

“Muundo huu ni sehemu ya taarifa ambayo ilipitishwa na CMSA kwa ajili ya kujiorodhesha DSE. Tangu kujisajili DSE kilichobadilishwa ni jina la Acacia kutoka African Barrick Gold Plc kuwa Acacia Mining Plc,” inasema taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Acacia wametangaza kufanya mkutano na wanahisa wake kwa mtandao kesho kutoa ufafanuzi zaidi juu ya sakata zima.

Walipofuatwa DSE kutoa maelezo ni kwa vipi kampuni ambayo haina usajili kuweza kujiorodhesha na kuuza hisa, walisema wao si wasemaji kwa kuwa mchakato wa kujiorodhesha huongozwa na kusimamiwa na CMSA na hivyo kumshauri mwandishi awasiliane nao.

Mwandishi alipowasiliana na  Ofisa Habari wa CMSA, Charles Shirima, alisema mtu aliyekuwa akishughulikia suala hilo alikuwa safarini Dodoma na kumtaka mwandishi awasiliane naye leo.

 

Bunge Latoa Azimio La Kuitaka Serikali Ichukue Hatua KALI Kwa Wahusika Wote wa Mikataba Mibovu ya Madini

Bunge limeitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaothibitika kuhusika kuliingizia Taifa hasara na kuwakosesha Watanzania fursa ya kufaidika na rasilimali za madini.

Hoja hiyo imetolewa leo Jumatano bungeni baada ya kamati iliyoundwa jana na Spika Job Ndugai kupata maoni ya namna Bunge linavyoweza kuunga mkono juhudi binafsi zinazochukuliwa na Rais John Magufuli kukabiliana na udanganyifu unaofanywa kwenye sekta hiyo.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Newala Mjini, George Mkuchika baada ya kukamilisha taratibu zote, imetoa maazimio matatu ambayo yamepitishwa na Bunge.

"Bunge linamuunga mkono Rais John Magufuli na lipo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kadri itakavyohitajika kuhakikisha juhudi hizi hazipotei bure na sekta ya madini inachangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla," amesema Mkuchika.

Kukubaliana na kinachofanywa na Rais Magufuli maazimio matatu yametolewa ambayo ni kumpongeza na kuunga mkono kwa hatua anazochukua, kumhakikishia ushirikiano wakati wowote atakapohitaji na kushauri kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kushiriki kulitia taifa hasara kutokana na kuidhinisha mikataba mibovu na wizi uliofanywa.

 

Acacia wakutana na Rais Magufuli Ikulu leo, wakubali kulipa fedha wanazodaiwa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.

Prof. John L. Thornton ambaye amesafiri kwa ndege binafsi kutoka nchini Canada hadi Tanzania amekutana na Mhe. Rais Magufuli leo Juni 14, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam na mazungumzo yao yamehudhuriwa na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.

Baada ya Mazungumzo hayo Prof. John L. Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili.

Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof. John L. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amevionya vyombo vya habari vinavyowataja Marais wastaafu Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na kuwahusisha na taarifa za kamati mbili za uchunguzi wa madini yaliyo katika makontena yenye mchanga wa madini (Makinikia) ambao ripoti zimekabidhiwa kwake na kamati hizo.

“Nimesoma ripoti zote mbili hakuna mahali ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete wametajwa, vyombo vya habari viache kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa letu, viwaache wapumzike” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Juni, 2017

SEARCH BLOG